Saturday, July 13, 2013

Tangazo kutoka sekretarieti ya ajira serikalini

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu 29 (1). Jukumu la msingi la Sekretarieti ya Ajira ni kuendesha mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma. Hapa ina maana kuwa jukumu la kuajiri, kuthibitisha watumishi kazini pamoja na masuala ya nidhamu ya Watumishi yanabaki kwa Watendaji Wakuu wa Wizara na Taasisi katika Utumishi wa Umma mitarafu ya Kifungu cha 6(1) (b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma no 8 ya mwaka 2002. Ambapo katika kuendesha mchakato huo, Sekretarieti ya Ajira inapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, na Taratibu zilizopo ili kuhakikisha Utumishi wa Umma unapata Watumishi weledi na wenye maadili mema. Ambapo hadi sasa jumla ya waombaji 4891 tumeshaendesha mchakato wao wa ajira na kuwapangia vituo vya kazi.
Hata hivyo, Sekretarieti ya Ajira kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ilipeleka Mswada Bungeni unaopendekeza kukasimu madaraka ya kuendesha mchakato wa Ajira ili baadhi ya Waajiri wakasimiwe madaraka hayo ili kurahisisha utendaji kazi katika kushughulikia mchakato wa ajira kwa baadhi ya kada. Huku Sekretarieti ya Ajira ikiendelea kuhakikisha kuwa jukumu hilo linaendelea kutekelezwa kwa ufanisi. Tunapoongelea suala la ufanisi hapa Kitengo cha Udhibiti na Ubora kinasimamia suala zima la uhakiki wa taarifa za mhusika, uhakiki wa vyeti na uadilifu wake kwa ujumla. Ambapo hadi sasa tumeshabaini jumla ya vyeti vya kughushi 677 ambavyo wahusika wanadai wamevipata kutoka RITA, VETA na NECTA.
Nafasi wazi za kazi zitakazokuwa zikitangazwa na mchakato wake kuweza kukasimiwa ni pamoja na Kada ya Wasaidizi wa ofisi, Wahudumu wa afya, Madereva, Maafisa Watendaji wa Kata, Mtaa, Kijiji, Wapishi, Walinzi, Madobi, Wasaidizi watunza kumbukumbu pamoja na Makatibu Muhtasi (walio chini ya cheo cha mwandishi mwendesha ofisi) au Kada zingine ambazo Katibu wa Sekretarieti ataona inafaa kukasimu.
1Aidha, nitoe ushauri kwa wanafunzi walioko shuleni na wanaotarajia kuingia vyuoni kuchukua masomo ama kozi za fani ya Afya, Elimu, Mifugo na Kilimo maana ni maeneo ambayo bado yana fursa nyingi za ajira Serikalini na wahitimu wake pindi wamalizapo wanapangiwa vituo vya kazi moja kwa moja bila ya kupitia mchakato wetu wa ajira kutokana na uhaba wa Wataalam wa fani hizo katika soko la ajira hivi sasa.
Sekretarieti ya Ajira katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kwa haraka zaidi zinazohusu mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma, pamoja na kuboresha mawasiliano kati ya Ofisi yetu na wadau ili kuweza kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya habari na mawasiliano nchini na duniani kwa ujumla, iliamua kuanzisha tovuti yake (www.ajira.go.tz) ambayo imerahisisha kwa kiasi kikubwa utoaji na upokeaji wa taarifa mbalimbali hususani za matangazo ya fursa za ajira taarifa nyingine zinazohusu masuala ya ajira Serikalini na matangazo mengine yanayohusu shughuli za Sekretarieti ya Ajira. Tangu kuzinduliwa mwezi Aprili, 2012 imeweza kutembelewa na wadau wapatao 3,017,410
Pamoja na tovuti Sekretarieti ya Ajira imeanzisha KANZIDATA (DATABASE) za aina tatu (3) ambazo ni Kanzidata ya Wahitimu wa Vyuo na Watalaam weledi, Kanzidata ya waliofaulu usaili na Kanzidata ya waliopangiwa vituo vya kazi.
Jambo lingine ambalo ningependa mkalifahamu ni kuwa, Sekretarieti ya Ajira iko katika hatua za awali za mchakato wa kuwawezesha waombaji wa fursa za ajira kuwasilisha maombi ya kazi kwa mfumo wa kielektroniki (e-application) kwa nafasi wazi zitakazokuwa zikitangazwa katika Utumishi wa Umma ili kurahisisha kupunguza mlolongo wa uendeshaji mchakato wa ajira ulivyo hivi sasa.
Mwisho nimalizie kwa kuwataka waombaji wa fursa za ajira kutokuchagua maeneo ya kufanyia kazi, hususani wale wanaopangiwa vituo vya kazi na Sekretarieti ya ajira na hawaendi kuripoti bila ya kutoa sababu za msingi maana Sekretarieti ya Ajira inaona hili ni kosa na inaandaa utaratibu wa kutowaruhusu kufanya usaili mwingine waombaji kama hao.



Imetolewa tarehe 12 Julai, 2013 na Riziki V. Abraham, Msemaji na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma +255-68762497

No comments:

Post a Comment