Thursday, July 11, 2013
Mafuta ya Oki, Viking, Asma sasa marufuku
Shirika la Viwango (TBS) limepiga marufuku uuzaji, ununuzi na matumizi ya mafuta ya kula ya aina ya Oki, Viking na Asma baada ya kubainika kuwa hayana ubora na hatari kwa afya za watumiaji.
Kwa mujibu wa Tangazo lilitolewa na Shirika la Viwango nchini (TBS) kwa baadhi ya vyombo vya habari jana, yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009.
Tangazo hilo lilisema TBS ilinunua mafuta hayo yanayozalishwa nchini Malayasia na kuingizwa kupitia njia za panya, kusambazwa sokoni na kubainika kuwa hayajakidhi matakwa ya kiwango cha kimataifa TZS 559:2010 kinachotumiwa nchini.
“Matokeo ya uchunguzi wa sampuli zake yalibainika kuwa yameshaharibika kabla ya kufikia ukomo wa matumizi kutokana na kutosafishwa ipsavyo, ni machafu kutokana na kuchanganyika na maji hivyo vigezo vya ubora wa mafuta havikufikiwa.”
Kwa msingi huo, TBS imewataka wauzaji wa mafuta hayo kuyaondoa sokoni mara moja na wateja kuacha kuyanunua hadi hapo itakapothibitika kuwa yamefikia kiwango kinachotakiwa.
Awali NIPASHE ilichunguza na kubaini kuwa mafuta hayo hushushwa kwenye bandari bubu ya ufukwe wa Mbweni jijini Dar es Salaam na wafanyabiashara ambao pia walidaiwa kukwepa kulipa ushuru.
Kazi hiyo hufanywa bila kificho na baadhi ya waliozungumza na mwandishi wetu walieleza kuwa huenda kuna ushirikiano na maofisa wa vyombo vya dola wasio waaminifu.
Licha ya kukwepa kodi, pia mafuta hayo yamekuwa yakiuzwa kwa bei ya chini kati ya Sh. 38,000 na 45,000 kwa ujazo wa lita 20 na kuwaumiza wazalishaji wa mafuta ya ndani ambao huuza mafuta ya ujazo huo kwa kati ya Sh. 52,000 na 55,000.
Tofauti hiyo husababisha wenye viwanda vya ndani kushindwa kufanya biashara kutokana na mafuta hayo kukosa mshindani na kuzagaa sokoni.
Mafuta hayo yamekuwa yakitumiwa kwa wingi na wafanyabiashara hasa wakaanga chipsi kwa vile ndiyo mafuta ya bei nafuu.
CHANZO: NIPASHE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment