Sekretarieti ya Ajira
katika Utumishi wa Umma ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya
Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na.
18 ya mwaka 2007 kifungu 29 (1). Jukumu la msingi la Sekretarieti ya
Ajira ni kuendesha mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma. Hapa ina
maana kuwa jukumu la kuajiri, kuthibitisha watumishi kazini pamoja na
masuala ya nidhamu ya Watumishi yanabaki kwa Watendaji Wakuu wa Wizara
na Taasisi katika Utumishi wa Umma mitarafu ya Kifungu cha 6(1) (b) cha
Sheria ya Utumishi wa Umma no 8 ya mwaka 2002. Ambapo katika kuendesha
mchakato huo, Sekretarieti ya Ajira inapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni,
na Taratibu zilizopo ili kuhakikisha Utumishi wa Umma unapata Watumishi
weledi na wenye maadili mema. Ambapo hadi sasa jumla ya waombaji 4891
tumeshaendesha mchakato wao wa ajira na kuwapangia vituo vya kazi.
Hata hivyo, Sekretarieti
ya Ajira kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa
Umma ilipeleka Mswada Bungeni unaopendekeza kukasimu madaraka ya
kuendesha mchakato wa Ajira ili baadhi ya Waajiri wakasimiwe madaraka
hayo ili kurahisisha utendaji kazi katika kushughulikia mchakato wa
ajira kwa baadhi ya kada. Huku Sekretarieti ya Ajira ikiendelea
kuhakikisha kuwa jukumu hilo linaendelea kutekelezwa kwa ufanisi.
Tunapoongelea suala la ufanisi hapa Kitengo cha Udhibiti na Ubora
kinasimamia suala zima la uhakiki wa taarifa za mhusika, uhakiki wa
vyeti na uadilifu wake kwa ujumla. Ambapo hadi sasa tumeshabaini jumla
ya vyeti vya kughushi 677 ambavyo wahusika wanadai wamevipata kutoka
RITA, VETA na NECTA.
Nafasi wazi za kazi
zitakazokuwa zikitangazwa na mchakato wake kuweza kukasimiwa ni pamoja
na Kada ya Wasaidizi wa ofisi, Wahudumu wa afya, Madereva, Maafisa
Watendaji wa Kata, Mtaa, Kijiji, Wapishi, Walinzi, Madobi, Wasaidizi
watunza kumbukumbu pamoja na Makatibu Muhtasi (walio chini ya cheo cha
mwandishi mwendesha ofisi) au Kada zingine ambazo Katibu wa Sekretarieti
ataona inafaa kukasimu.
1Aidha, nitoe ushauri
kwa wanafunzi walioko shuleni na wanaotarajia kuingia vyuoni kuchukua
masomo ama kozi za fani ya Afya, Elimu, Mifugo na Kilimo maana ni maeneo
ambayo bado yana fursa nyingi za ajira Serikalini na wahitimu wake
pindi wamalizapo wanapangiwa vituo vya kazi moja kwa moja bila ya
kupitia mchakato wetu wa ajira kutokana na uhaba wa Wataalam wa fani
hizo katika soko la ajira hivi sasa.
Sekretarieti ya Ajira
katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kwa haraka zaidi zinazohusu
mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma, pamoja na kuboresha
mawasiliano kati ya Ofisi yetu na wadau ili kuweza kuendana na
mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya habari na mawasiliano nchini na
duniani kwa ujumla, iliamua kuanzisha tovuti yake (www.ajira.go.tz)
ambayo imerahisisha kwa kiasi kikubwa utoaji na upokeaji wa taarifa
mbalimbali hususani za matangazo ya fursa za ajira taarifa nyingine
zinazohusu masuala ya ajira Serikalini na matangazo mengine yanayohusu
shughuli za Sekretarieti ya Ajira. Tangu kuzinduliwa mwezi Aprili, 2012
imeweza kutembelewa na wadau wapatao 3,017,410
Pamoja na tovuti
Sekretarieti ya Ajira imeanzisha KANZIDATA (DATABASE) za aina tatu (3)
ambazo ni Kanzidata ya Wahitimu wa Vyuo na Watalaam weledi, Kanzidata ya
waliofaulu usaili na Kanzidata ya waliopangiwa vituo vya kazi.
Jambo lingine ambalo
ningependa mkalifahamu ni kuwa, Sekretarieti ya Ajira iko katika hatua
za awali za mchakato wa kuwawezesha waombaji wa fursa za ajira
kuwasilisha maombi ya kazi kwa mfumo wa kielektroniki (e-application)
kwa nafasi wazi zitakazokuwa zikitangazwa katika Utumishi wa Umma ili
kurahisisha kupunguza mlolongo wa uendeshaji mchakato wa ajira ulivyo
hivi sasa.
Mwisho nimalizie kwa kuwataka waombaji
wa fursa za ajira kutokuchagua maeneo ya kufanyia kazi, hususani wale
wanaopangiwa vituo vya kazi na Sekretarieti ya ajira na hawaendi
kuripoti bila ya kutoa sababu za msingi maana Sekretarieti ya Ajira
inaona hili ni kosa na inaandaa utaratibu wa kutowaruhusu kufanya usaili
mwingine waombaji kama hao.
Imetolewa tarehe 12
Julai, 2013 na Riziki V. Abraham, Msemaji na Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika
Utumishi wa Umma +255-68762497
No comments:
Post a Comment